Ilichofanya Rwanda kuboresha dawa za asili

Na Flora Harrison

RWANDA iko katika mkakati wa kupunguza bidhaa inazoagiza nje ili kuboresha sekta mbalimbali za kiuchumi kwa kuhakikisha kwamba sasa baadhi ya bidhaa hizo zinazalishwa ndani.

Mkakati huo wa kuboresha soko la ndani kwa kuangalia bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa nchini humu unalenga pia kupunguza pengo la biashara ya kimataifa lililopo ambalo nchi zilizoendelea ndizo hufaidika zaidi, hatua ambayo pia itapunuza kiwango cha pesa ambacho Rwanda inatumia katika kuagiza bidhaa nje.

Mpango huo unatazamiwa kuendeshwa na vituo vya kijamii vya uchakataji na usindikaji bidhaa (CPCs) chini ya Mamala ya Taifa ya Maendeleo ya Viwanda na Utafiti (NIRDA). Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Maendeleo cha NIRDA, Dk George Nyombaire, mamlaka hiyo kwa sasa inaendesha miradi kwa kufungua vituo nchi mzima ambako dawa zinazotokana na mitishamba (pia hujulikana kama dawa za asili, jadi au za kienyeji) zitakuwa zinafanyiwa utafiti ili baadaye zizalishwe viwandani.

Mpango huo unalenga kuongeza ubora wa dawa hizo ili kuifanya sekta hiyo kuwa ya ushindani na iliyoboreka zaidi, Nyombaire anasema. “Mpango huo unajielekeza katika kuboresha mchakato wa uzalishaji wa dawa za asili kwa kuzingatia mbinu za kisasa, hatua ambayo itaongeza na kuimarisha ushindani wa bidhaa zinazotokana na mitishamba,” anasema Nyombaire.

Ofisa huyo anasema serikali itawapa watafiti wa dawa za asili na waganga wa jadi ujuzi wa namna ya kutayarisha bidhaa zao kwa ajili ya kuzalishwa katika viwanda, hatua ambayo anasema itasaidia pia kuboresha ubora pamoja na mlolongo wa thamani.

Mpango wa kuboresha bidhaa zinazotokana na dawa za asili nchini Rwanda (phytomedicine) umetengewa Faranga za Rwanda milioni 630 (Shilingi bilioni 1.6) ambazo ni msaada ya kutoka Ubelgiji.

Mbali na watafiti wa NIRDA, mpango huo unaotarajiwa kukamilika mwaka 2020, pia unasimamiwa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Rwanda na Wizara ya Afya.

KUFUATA NYAYO ZA CHINA, INDIA

Tayari NIRDA imeanza mafunzo kwa watafiti wa dawa za asili na waganga wa jadi waliosajiliwa na kuwataka kuimarisha uzalishaji wa dawa zao. Hivi karibuni, mamlaka hiyo iliwapiga msasa watafiti 82 wa mitishamba kupitia mafunzo maalumu.

Takwimu zinaonesha kuwa kuna takribani watafiti na waganga wa jadi 3,000 waliosajiliwa nchini kote, na ambao hawajasajiliwa ni takribani 14,000. “Vituo vya uchakataji na usindikaji vitakuwa na uwezo wa kutengeneza dawa zitokanazo na mitishamba zinazofikia viwango, kuziweka katika vifuniko sahihi na kuziwekea alama na lebo kama wanavyofanya wenzetu wa China, Korea ya Kusini na India,” Nyombaire anasema.

Anaongeza kuwa pia dawa hizo zitakuwa na maelezo kwa wagonjwa kwa maana ya vipimo (dosage) na matumizi, na pia zitaonesha mchanganyiko uliomo (ingredients) na tarehe ya kumalizika kwa matumizi. “Hii itasaidia maendeleo ya sekta ya afya na pia kufanya sekta hiyo kuwa na faida zaidi,” anasema.

Kuboresha mchakato wa uzalishaji wa dawa za mitishamba kwa viwango vya kimataifa na uzalishaji wa mbolea zisizo na kemikali ni baadhi ya miradi ya kipaumbele ya NIRDA iliyoanzishwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Ikumbukwe kwamba sheria ambayo ilianzisha NIRDA inaipa uwezo mamlaka hiyo kuunda kampuni ambayo inaweza kufanya kazi katika ngazi ya kiwanda. Kwa hiyo, vituo vya uchakataji na usindikaji vinafanya kazi chini ya mkakati huu kwamba muda wowote vinaweza kuwa viwanda kamili vya kuzalisha dawa.

KUZALISHA AJIRA

Prof Michel Frederich kutoka Chuo Kikuu cha Liege nchini Ubelgiji, ambacho kinausaidia mradi huo kusimama, anasema kuendeleza sekta ya waganga wa jadi na watafiti wa dawa za asili ni mpango ambao utasaidia kutengeneza ajira nyingi kuanzia uzalishaji hadi usambazaji, Mradi huo unaojulikana kwa Kifaransa ‘Optimization de la pharmacopee traditionnelle Rwandaise’ ambao tafsiri yake isiyo rasmi inaweza kuwa ‘Uboreshaji wa dawa za jadi za Rwanda’, unahusisha matumizi ya dawa za jadi kwa kuzizalisha kitaalamu na hivyo kueleza vitu vyote muhimu vilivyomo, matumimzi na hata madhara (side effects) kama ilivyo kwa dawa za kisasa.

“Tulianzisha mradi huu kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Rwanda mwaka jana ili kuboresha ubora wa dawa za asili. Tuliwapa mafunzo watu watatu katika NIRDA, wawili kutoka Chuo Kikuu cha Rwanda na mwanasayansi jamii mmoja.

“Pia tunatumia mradi huu kutoa taarifa muhimu kwa wanafunzi wanaosomea udaktari wa falasafa (PhD) kuhusu dawa za asili, na mafunzo ya sasa ya wataalamu wa dawa za asili ni sehemu ya Faranga milioni 630 zilizotolewa kwa ajili ya mradi,” anasema Akizungumza baada ya mafunzo ya wataalamu wa tiba asilia hivi karibuni jijini Kigali, Prof Frederich anasema sehemu ya tatu ya mradi itahusisha kuandaa na kuboresha dawa za asili kutoka kwenye mimea, kuhakikisha ubora katika usindikaji, kusimamia vipimo (dosage), kuimarisha mchakato wa uzalishaji, na kusaidia watu kufanya biashara ya kuzalisha mimea tiba.

Mchakato huu, anaongeza, utasaidia kutengeneza fursa za ajira katika sekta hiyo, akibainisha kuwa ni bora kuzalisha dawa zitokanazo na mitishamba ndani ya nchi badala ya kutegemea kuagiza nje kila dawa.

Anasema kwamba uendelezaji wa viwanda ni mojawapo ya vipengele muhimu vya Mkakati wa pili wa Maendeleo ya Kiuchumi na Mkakati wa Kupunguza Umasikini (EDPRS II) wa

Rwanda, na kwamba serikali imejipangia kutengeneza ajira 200,000 kila mwaka.

KULINDA MIMEA TIBA ISITOWEKE

Dk Nyombaire (pichani) anasema serikali inahimiza utunzaji na ulimaji miti inayotoa dawa kwa binadamu iliyo katika hatari ya kutoweka. Anaongeza kuwa hivi karibuni serikali itatenga maeneo ya ardhi katika wilaya mbalimbali kwa ajili ya kupanda mimea ya dawa iliyo katika hatari ya kutoweka.

“Mbali ya kulinda mimea inayotumika kuzalisha dawa ambayo iko katika hatari ya kutoweka na kuitumia kuzalisha dawa viwandani, tumepanga kuwapeleka waganga wa jadi na watafiti katika ziara za kujifunza kwenye nchi nyingine zilizoendelea katika kutengeneza dawa za mimea ili wazidi kujifunza kwa vitendo kutoka kwa wenzao.

Tunataka kuona dawa za asili zinazozalishwa Rwanda zikiuzwa katika soko la kimataifa. Hata hivyo, chama cha wataalamu wa tiba za asili cha AGA Rwanda Network, kinasema kinahitaji Faranga milioni 416 ili kurejesha mimea tiba iliyo katika hatari ya kutoweka katika nchi hiyo ndogo.

Kundi hilo linasema kuna aina zaidi ya 700 ya miti ya dawa ambayo iko katika hatari kubwa ya kutoweka nchini Rwanda. Daniel Gafaranga, Rais wa chama hicho, anasema mtandao wao umepania kuokoa mimea inayotoa dawa.

Anawahimiza waganga wa jadi na watafiti wa mitishamba kulinda miti isitoweke na hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia nchi. MSAADA WA SERA Edmond Semana, Ofisa wa Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya uthamini na usajili anasema sheria inayozungumzia tiba za asili na mitishamba kwa ujumla inafanyiwa marekebisho baada ya kutoa katika tume ya marekebisho ya sheria.

Semana anasema sheria hiyo iliwasilishwa hivi karibuni kwenye Baraza la Mawaziri na anaamini haitachukua muda kabla kufikishwa bungeni ili kujadiliwa na kuwa sheria kamili. “Hii ni mara ya kwanza tunatengeneza sheria kama hiyo nchini Rwanda, ambayo pia itaanzisha Baraza la Taifa la Waganga wa jadi na Watafiti wa Dawa Asilia,” anasema

Advertisements

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s