Kuwa Mwanafunzi Dar… Yataka Moyo

NA ESTHER STEVEN

UKIJARIBU kufuatilia wanafunzi wanaopata shida katika maisha yao ya kutafuta elimu, basi wanafunzi wanaosoma shule za misingi na wanafunzi walio na umri mdogo huteseka sana.

Lakini wanafunzi wanaoteseka zaidi ni wale waliopo Jijini Dar es Salaam, na wanaishi mbali na shule wanazosoma.

Mara nyingi haswa nyakati za asubuhi na jioni huwa naumia nikiwaona watoto wadogo wa shule za msingi wakihangaika kupigania usafiri ili waweze kuwahi shuleni au majumbani kwao.

Swali ambalo mara nyingi nilikuwa nikijiuliza ni kuwa huko wanakoishi hakuna shule mpaka wagombanie usafiri kuelekea shule zilizopo mbali na makazi yao?

Mfano kuna wanafunzi wa shule ya msingi ya Diamond (wilaya ya Ilala) lakini wanaishi Mwenge, wengine wanasoma shule ya msingi Mtendeni (wilaya ya Ilala)  wanaishi Kawe, vilevile kuna wanafunzi wa shule ya msingi ya Muhimbili ambao wanaishi JKT.

Mbali na hao wanafunzi wao, pia wapo wengine wengi wanaosoma shule za mbali na wanakoishi wapo wanaoishi Kunduchi na wanasoma Mwenge, lakini jambo la kushangaza huko wanapoishi kuna shule nyingi tena zakutosha.

Lakini katika safari zao kuelekea shuleni au nyumbani hukumbana na mikikimiki na misukosuko mingi ambayo kwa kiasi kikubwa huwa ni changamoto katika maisha yao ya kielimu.

Changamoto hizo ni pamoja na kusubiri daladala kwa mda mrefu ambapo hali hii hupelekea wanafunzi kuchelewa shuleni na kushindwa kuhudhuria baadhi ya vipindi ambavyo vinafundishwa asubuhi.

Vilevile ndani ya daladala wanafunzi hawa hubanana sana, hii hutokana na uwepo wa abiria wengi ndani ya daladala na pia ni hatari kwa wanafunzi wenye umri mdogo kwani hata kupata usafiri inakuwa ni shida sana.

Mbali na hayo, wanafunzi husimama kwa mda mrefu kutokana na umbali uliopo kutoka majumbani kwao mpaka shuleni, mfano mwanafunzi anaeishi JKT na anasoma shule ya msingi Muhimbili atalazimika kusimama kwa mda wa saa 1 mpaka kufika shuleni.

Kwa hali kama hii utamkuta mwanafunzi amechoka sana hata akifanikiwa kuwahi vipindi vya asubuhi bado hataweza kuelewa kwani anahitaji apate mda kwa kupumzika ili kuondoa uchovu wa safari, lakini nafasi hiyo hawezi kuipata kutokana na kuchelewa.

Ukiachia mbali uchovu anaokuwa nao mwanafunzi  huyo, bado ataandamwa na adhabu za hapa na pale kwa sababu ya kuchelewa kwake shule au kuchelewa kipindi darasani.

Pia katika baadhi ya daladala, makondakta huwakataza wanafunzi wasipande kutokana na usumbufu wanaokuwa nao, kwani wengi wao hudai wamepoteza hela za nauli.

Mara kadhaa nimewahi kuwasikia wanafunzi wakiomba nauli kwa watu mbalimbali wanaokuwa katika vituo vya daladala ili waweze kurudi nyumbani, wengine wanalia sana wakidai wameibiwa au wamepoteza nauli zao.

Suala hili linatakiwa liangaliwe sana na wazazi, kwani wao huwachagulia watoto wao shule zilizopo mbali bila kujua changamoto wanazozipata katika safari zao za kila siku kuelekea shuleni.

Mara nyingi utasikia wazazi wakilalamikia matokeo mabaya ya watoto wao na kuwalaumu walimu, kumbe wao ndio chanzo kikubwa cha matokeo mabaya, kwani hawawezi hata kufatilia maendeleo ya watoto wao.

Hivyo basi badala ya kuwatupia lawama walimu huko mashuleni, wazazi hakikisheni mnawaandikisha watoto wenu katika shule zilizipo karibu na makazi yenu ili muweze kufatilia maendeleo yao shuleni.

Pia ipo haja ya serikali kufanya utafiti katika shule zote ili kujua ni wanafunzi wangapi wanaoishi mbali na makazi yao na kuona ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto hawa kupata elimu bora bila kukumbana na changamoto nyingi ambazo wametengenezewa na wazazi.

Advertisements

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s